Ni kauli za watu ambao wako katika mahusiano ya kimapenzi.
Lakini siyo kweli, eti kwamba huwezi kuishi bila yeye kwa sababu yeye ndiyo kila kitu kwako.
Alikuambia nani dunia iko hivyo?
Usipende kujipa vizuizi vingi kwenye maisha yako, maisha tayari ni magumu na wewe unayafanya kuwa magumu zaidi kwa kujiongezea mzigo kwamba huwezi kuishi bila yeye.
Mtu anapokuwa kwenye hisia za mapenzi ni rahisi sana kutamka maneno hayo lakini kiuhalisia siyo kweli. Unaweza kuishi bila yeye, na wengine wanakuwa wanasema maneno hayo ili waweze kupata kile wanachotaka, hayo yanakuwa ni maneno ya kutaka tu kuteka hisia za mtu.
Leo nataka nikupe sababu moja tu kwanini unaweza kuishi bila yeye na kujiondoa kwenye vifungo vya maisha, ukishajua hii sababu acha kuifunga akili yako na uone mambo katika uhalisia wake.
Siwezi kuishi bila yeye kwa sababu yeye ndiyo kila kitu kwangu, siyo kweli unaweza kuishi bila yeye kwa sababu yeye siyo pumzi yako.
Kitu pekee ambacho huwezi kuishi bila kuwa nacho ni pumzi tu. Ni wangapi walishawahi kusema hivyo hawawezi kuishi bila mtu fulani lakini kwa sasa mbona wanaishi bila wao?
Tunakua na watu wetu wa karibu ambao tunawapenda sana siku wakiondoka duniani tunalia sana na baada ya muda unasahau na maisha yanaendelea na hapo aliyeondoka anakuwa hajaondoka na pumzi yako.
Mtu akikuambia siwezi kuishi bila wewe, mwambie siyo kweli, kitu pekee ambacho siwezi kuishi bila hicho ni pumzi tu.
Ukimkosa mtu fulani au kitu fulani huwezi kufa lakini ukikosa pumzi, utakufa.
Wako watu ambao wanajipa mamlaka ya juu sana utafikiri wao ndiyo pumzi au Mungu kwamba bila mimi, wewe huwezi kuishi, bila mimi hapa kazini mambo hayaendi rafiki yangu, dunia ina utele hata aondoke nani mambo yataendelea. Hakuna mtu ambaye anaweza kusimamisha dunia hata siku moja.
Wewe ni muhimu sana kwenye hii dunia lakini ni kama tone dogo tu katika maji ya bahari hivyo usiwe unawatisha watu kwamba hawezi kufanya kitu fulani bila wewe. Dunia inaweza kuendelea bila hata ya wewe, hivyo ishi kwa hekima na unyenyekevu kwamba wengine wanaweza kufanya bila wewe na wengine wanaweza kuishi bila wewe usijipe mamlaka ya kimungu wakati wewe ni binadamu.
Hatua ya kuchukua leo; kitu pekee ambacho huwezi kuishi bila kuwa nacho ni pumzi, hivyo acha kujipa vizuizi ambavyo havina maana unaweza kuishi na kuendelea na maisha yako kama ukiwa na pumzi tu.
Ondoka kwenye utumwa wa kitu chochote kile, iwe ni mapenzi, kazi, biashara, huduma nk. Usiendelee kuvitukuza vitu na kujishikiza kwenye vitu hivyo kwamba maisha yako hayawezi kwenda bila kuwa na vitu hivyo. Kwa mfano, unahofia kufukuzwa kazi au kupoteza kile ulichopanga kwamba ukipoteza hivyo basi maisha yako hayawezi kwenda, maisha yako yanaweza kwenda vizuri tu kama ukiwa na pumzi. Acha kujidanganya na vitu vingine.
MUHIMU;
Kama bado hujajiunga na kundi la wasapu la Mimi ni Mshindi jiunge leo kwani kuna maarifa mengi unayakosa ambayo sikushirikishi hapa.
Kujua ni maarifa gani hayo na jinsi ya kujiunga nitumie ujumbe wasapu kwa namba 0717101505. Kupata vitabu vizuri vya kujisomea kwa lugha ya kiswahili wasiliana kwamba namba 0717101505.
Rafiki Na Mwalimu Wako, Afisa Mhamasishaji Mkuu (CIO)Chief Inspiration Officer.
Mwl. Deogratius Kessy
0717101505//0767101504
https://kessydeo.home.blog