Ni macho na masikio.
Macho yako wewe kama una biashara yanatakiwa kuwa kwenye namba. Unapaswa kujua namba muhimu za biashara yako kama vile mtaji unaozunguka kwenye biashara, idadi ya mauzo kwenye biashara, faida unayopata na kuhakikisha biashara yako inatengeneza masoko mapya kila siku.
Huwa tunajinyima fedha nyingi kwenye biashara kwa sababu ya biashara kutokujulikana na wateja, hivyo kazi yako kubwa kwenye biashara kutengeneza masoko kwa sababu masoko ndiyo yanaleta mauzo na mauzo ndiyo yanaleta fedha kwenye biashara.
Masoko ni kitu muhimu sana katika biashara yako.
Masoko ni kuiwezesha biashara yako kujulikana, watu waijue biashara unayoifanya na wajue uwepo wako. Kwenye masoko hutakiwi kusimama maana ukisimama tu utaleta msiba kwenye biashara. Si unajua kile kitendawili kinachosema, hakisimami, kikisimama msiba, na jibu lake ni moyo. Kumbe basi, masoko ni kama moyo kwenye biashara, ukisimama biashara nayo inasimama na matokeo yake ni msiba.
Na biashara yoyote unayofanya hakikisha unapata faida, huwezi kuendesha maisha yako kwa hasara kwani hasara hazilipi bili bali faida ndiyo zinalipa bili.
Kiungo kingine ni masikio. Masikio yako yanapaswa kuwa kwa mteja.
Masikio kuwa kwa mteja ndiyo huduma kwa mteja. Na hapa kwenye huduma kwa mteja ndiyo kuna kazi kubwa sana, maana unaweza kufanya macho yako yawe kwenye namba lakini kama masikio yako hayapo vizuri kwenye huduma kwa mteja unakuwa unajipoteza mwenyewe kwenye biashara yako.
Masikio kwa wateja maana yake nini? Unapaswa kutoa huduma nzuri kwa wateja, kuanzia kumkaribisha mteja, kumsalimia, kumsaidia changamoto yake anayopitia na amekuja kwako ili apate suluhisho, mfanye ajisikie bora na kupata suluhisho pale anapopata huduma yako.
Msikilize mteja wako, mara nyingi mteja ndiyo bosi wako maana yeye ndiyo anayekuletea wewe fedha. Hivyo unapaswa kumsikiliza anataka nini na umpatie kile anachotaka.
Hata kama mteja unaona hajui kitu fulani, usimrekebishe kwa sababu wateja mara zote wako sahihi na huwa hawapendi kuonekana wanajua.
Waelezee wateja wako vizuri bidhaa anayopata kwako itakwenda kumsaidiaje. Usimwache mteja akiwa hajui la kufanya, mweleze na msaidie katika kutafuta kile anachotaka.
Hatua ya kuchukua leo; komaa na vitu hivi viwili kwenye biashara yako, macho yako kwenye namba na masikio yako kwa mteja.
Ukivifanyia kazi vitu hivyo, biashara yako itaenda vizuri. Leo nenda kawasikilize wateja wako hakikisha masikio yako yanakuwa kwa mteja na macho kwenye namba za biashara.
Usivipuuze vitu hivi maana ukipuuza biashara itaanguka.
MUHIMU;
Kama bado hujajiunga na kundi la wasapu la Mimi ni Mshindi jiunge leo kwani kuna maarifa mengi unayakosa ambayo sikushirikishi hapa.
Kujua ni maarifa gani hayo na jinsi ya kujiunga nitumie ujumbe wasapu kwa namba 0717101505. Kupata vitabu vizuri vya kujisomea kwa lugha ya kiswahili wasiliana kwamba namba 0717101505.
Rafiki Na Mwalimu Wako, Afisa Mhamasishaji Mkuu (CIO)Chief Inspiration Officer.
Mwl. Deogratius Kessy
0717101505//0767101504
https://kessydeo.home.blog