Rafiki,
Kila mmoja wetu anafanya makosa katika maisha yake.
Hakuna ambaye ni mkamilifu na asili ya kila binadamu ni kukosea, tunapokosea ndiyo huwa tunajifunza.
Maisha ni kama shule na changamoto tunazo kutana nazo ndiyo mitihani.
Kumbe basi, tunapokimbia changamoto maana yake hutaki kwenda darasa lingine bali unataka kubaki darasa hilo hilo yaani kama uko la tano ili uende la sita lazima ufanye kwanza mtihani.
Kuna matatizo mengi yanayotokea katika maisha yetu kwa sababu mbalimbali huenda ni kwa sababu ya ujinga, uzembe, uvivu na nk.
Sasa katika kila changamoto unayopata , tatizo lolote jiulize je umechangiaje katika hilo tatizo.
Kwenye kila changamoto uliyonayo kuna namna umechangia, labda watoto wako wamekuwa wanatabia mbaya, wanaiba, hawana nidhamu ukichunguza kwa makini wewe ndiyo utakua umechangia, kama mtoto anaiba huenda malezi yako ni hayapo.
Mtoto hafanyi vizuri shule huenda hata haumsaidii kwenye masomo yake. Hapo utaona ni namna gani na wewe umechangia kwa mtoto wako kuwa hivyo alivyo leo.
Labda kuna ajali imetokea na wewe ulikuwa ndani ya gari umeona kabisa dereva anaendesha kwa mwendokasi mkali lakini hujakemea na ajali ikatokea je hapo hujachangia?
Ukipata fedha unatumia yote hata hujiwekei akiba siku unapatwa na dharura unajikuta huna kitu unakimbilia kukopa na kukopa unanyimwa je hapo utakuwa hujachangia kutokea kwa tatizo?
Kwa kukosa kwako umakini katika kazi unajikuta unafanya uzembe wakati wa kazi halafu unazalisha matokeo ambayo hayana ufanisi je hapo hujachangia kutokea kwa tatizo? Je ungeweka umakini yangetokea hayo?
Hujali juu ya afya yako, mwili unadhoofika unapatwa na magonjwa je hapo utakuwa hujachangia kutokea kwa tatizo katika mwili wako ?
Hatua ya kuchukua leo; Angalia kwenye kila tatizo kuna namna umechangia kutokea kwa tatizo hilo.
Jua hilo na chukua hatua haraka.
Kwahiyo, kama unaona kwa mfano mtu anakuibia katika biashara yako jua wewe ndiyo umechangia kwa sababu hujaweka mifumo mizuri ya udhibiti wa fedha zako.
Kila la heri rafiki yangu,
Rafiki na mwalimu wako,
Mwalimu Deogratius Kessy
http://www.mtaalamu.net/kessydeo
Asante sana.