Mpendwa rafiki yangu,
Kwenye dunia ya leo kila mmoja anajua kila kitu. ujio wa mitandao ya kijamii umewafanya watu kuwa mafundi wa kila kitu hata kama siyo fundi wa kitu hiko atataka achangie kitu na kutoa maoni yake juu ya kile kitu.
Huwezi kujifunza kitu kutoka kwa wengine kama wewe ni mtu wa kujifanya unajua kila kitu kwenye maisha yako. yule ambaye anajifanya anajua kila kitu huwa anaangusha vibaya kwa sababu kiburi cha kujiona anajua ataona ya nini kujifunza wakati anajua kila kitu?
Aliyekuwa mwanafalsafa wa kiyunani Plato aliwahi kusema, hekima pekee anayoijua ni kwamba hajui kitu. Nakubaliana na Plato kwa sababu ukijiona hujui kitu utakuwa na moto wa kujifunza sana lakini ukishajiona unajua unaona huna jipya tena la kujifunza na hapo ndiyo watu wanapoanguka vibaya.
Kuwa tayari kujifunza kutoka kwa wengine, unapojifunza ndiyo unajua mambo mengi. Hata kama kitu unakijua jifanye hukijui ili uweze kuongeza maarifa mapya.
Unatakiwa kuwa msikilizaji mzuri wa kujifunza kutoka kwa wengine na kusoma hata vitabu. Kama unashindwa kusoma hata kitabu kimoja kwa mwezi basi utakua unajipunja sana katika ukuaji wa kiakili.
Hatuwezi kukua sisi wenyewe kama akili zetu hazitoweza kushiba maarifa. Maarifa yamekuwa msaada kwa watu wengi tangu enzi na enzi. Hivyo ni vizuri tukajifunza kwa wale watu bora wanaofanya vitu kuwa bora.
SOMA; Jinsi Ya Kumfahamu Mtu Mwenye Hekima Na Mjinga
Unaweza ukajifunza kutoka kwa kitu chochote kile. Kadiri ya asili ya dunia kila kitu unachokiona mbele yako kinaweza kukupa funzo. Uwe mnyenyekevu katika kujifunza na utajua mambo mengi sana.
Hatua ya kuchukua leo; hakuna anayejua kila kitu duniani, hivyo ukitaka kujua zaidi jifunze zaidi na chukulia kuwa hujui kitu.
Kwahiyo, ukitaka kujiona kama hujui vitu vingi anza kujifunza leo na utajiona hujui kitu chochote kile. Jifunze kama vile chakula kwako na siyo sumu.
Muhimu; kama bado hujajiunga na kundi la wasapu la mimi ni mshindi jiunge leo kwani kuna maarifa mengi unayakosa ambayo sikushirikishi hapa. Kujua ni maarifa gani hayo na jinsi ya kujiunga bofya hapa au nitumie ujumbe wasapu kwa namba 0717101505. Kupata vitabu vizuri vya kujisomea kwa lugha ya kiswahili bonyeza hapa.
Ukawe na siku bora sana rafiki.
Rafiki na mwalimu wako,
Deogratius kessy
0717101505/0767101504
deokessy.dk@gmail.com // kessydeo@mtaalamu.net
Asante sana.