Habari ya wakati huu mpendwa rafiki na msomaji wa mtandao wa Kessy Deo? Natumaini u buheri wa afya rafiki yangu na mpendwa msomaji wa mtandao huu. Napenda kutumia nafasi hii kukukaribisha tena katika makala yetu ya leo ili tuweze kujifunza wote kwa pamoja.
Katika makala yetu ya leo tutakwenda kujifunza kitu kinacholeta mpasuko wa kifamilia hususani katika malezi ya watoto. Wazazi na walezi wengi wamekuwa wakisababisha mpasuko katika familia kwa kuwagawa watoto kulingana na sababu mbalimbali. Je nini sababu inayopelekea mpasuko katika familia? Nakusihi karibu uweze kuambatana na mimi mpaka mwisho wa makala hii.
Kitu kinacholeta mpasuko wa familia katika malezi ya watoto na kuwagawa ni UPENDELEO WA WAZI. Upendeleo ni kitu kinachochangia kuleta mpasuko wa kifamilia kwa mfano mzazi anaonesha upendeleo wa wazi kwa mtoto ambaye ana akili za kidarasani na kusema huyu ndio mwanangu wa kipekee kwa sababu anafanya vizuri darasani na wengine kudharaurika kuonekana hawana maana.
SOMA; Mfahamu Adui Wa Kisasa Anayeharibu Familia Yako
Watoto wote ni sawa na unapaswa kuwapokea kadiri Mungu alivyokujalia unatakiwa kuwapa wote mapenzi sawa. Hutakiwi kuonyesha upendeleo kwa mtoto mmoja hii inachnagia kuigawa familia na watoto wengine kuonekana wao siyo kitu katika familia.
Mpendwa msomaji, hili tunaliona hata katika familia zetu unakuta Yule mtoto mwenye kipato kikubwa basi ndio wazazi wanaonesha kumpenda kuliko watoto wengine. unatakiwa kuwapenda watoto wote bila kujali uwezo wao wa kiuchumi au uwezo wa akili za kidarasani.
Wazazi wengine wanakosea sana katika malezi ya watoto kwa kuwapandikiza watoto mbegu ya chuki tokea wakiwa wadogo, kwa mfano, baba utamsikia akisema kwa mtoto Fulani kwa kuwa wewe ndio una akili darasani kuliko wenzako wewe ndio mwanangu wa kipekee na nyie wengine ni watoto wa mama. Unaona ni jinsi kwa kuchukulia mfano huu unavyoleta mpasuko katika familia.
SOMA; Haya Ndio Makosa Kumi Na Moja (11) Wanayofanya Wazazi Au Walezi Katika Malezi Ya Watoto
Katika familia kama wazazi hawatakiwi kuwagawa watoto na kusema huyu ndio wa kwangu kwa sababu ana akili na kusema kuwa Yule ndio ana uchumi mzuri basi ndio mtoto wangu wote ni wa kipekee. Unatakiwa kutoa upendo wa bila kujibakiza kwa watoto wote katika familia.
Hatua ya kuchukua leo, watoto ni zawadi kutoka kwa Mungu, hivyo unapaswa kuwapokea jinsi walivyo na wala usibague kwa sababu zozote zile. Wapatie wote haki sawa zinazostahili kwa mtoto bila ubaguzi. Upendeleo wa wazi huleta mpasuko katika familia.
SOMA;Fahamu Kitu Muhimu Ambacho Familia Yako Inakosa
Kwa kuhitimisha, kama wazazi wanatakiwa kuondokana na dhana potofu ya kuwagawa watoto kulingana na mitazamo ya kizamani inayotumiwa na jamii nyingi. Usiwabague watoto wape kile wanachostahili bila upendeleo ili kuepuka mpasuko wa kifamilia. Tuishi katika mitazamo chanya kwa ajili ya familia zetu, jamii na taifa kiujumla. Kumbuka ili tuwe na jamii bora tunapaswa kwanza kujenga familia bora.
Mpendwa rafiki na msomaji wa mtandao wa Kessy Deo, nakutakia utekelezaji mwema katika haya uliyojifunza leo. Ili tuendelee kuwa pamoja zaidi kila siku penda kutembelea ukurasa wetu wa facebook na jiunge hapa na mtandao wetu kwa kubonyeza maandishi yaliyokolezwa.
Asante sana
Rafiki na mwalimu wako,
Deogratius Kessy
0717101505/0767101504 au deokessy.dk@gmail.com