Design a site like this with WordPress.com
Get started

Mambo Muhimu Unayoweza Kujifunza Kutoka Katika Kitabu Cha 5 Love Language

Habari mpendwa rafiki na msomaji wa mtandao wa Kessy Deo? Natumaini unaendelea vizuri na hongera kwa zawadi ya siku hii ya leo. Tumia muda
Mambo 20 niliyojifunza katika kitabu cha 5 Love Language kilichoandikwa na Gary Champman na Ross Campbell ni kama ifuatavyo;
1. Watoto wanahitaji upendo usiokuwa na kipimo. Watoto wanahitaji kujaziwa tank lao la upendo kama ilivyokuwa kwa watu wengine wanavyohitaji upendo.
Kama wewe ni mzazi jaza tanki la Upendo kwa mwanao. Upendo huvumilia yote.

2. Watoto wanahitaji kuhamasishwa na kutiwa moyo katika masomo yao.
Mwalimu wa kwanza katika malezi ni mzazi.
Usisubiri mtu mwingine amtie moyo mtoto wako kabla ya wewe.
Mpe matumaini kwenye kile anachofanya mtoto wako.

3. Madhara ya kutomuonesha mtoto hisia za upendo ni kubwa sana.
Mtoto Akikosa upendo kwa wazazi wake anahisi hata duniani siyo sehemu salAma ya yeye kuishi. Ni rahisi kujiingiza katika makundi hatarishi ambayo yatakuja kuathiri maisha yake

4. Changamoto kubwa ya wazazi siku hizi ni kujishughulisha zaidi na mambo ya kiuchumi na kusahau malezi ya watoto.
Wasaidizi wengi wa ndani siku hizi ndio wamekuwa wahanga wakubwa na kupewa nafasi kulea watoto.
Usipopanda mbegu ya upendo kwa mtoto wako usitegemee kuvuna mbegu ya upendo kwa watoto.

5. Mzazi anawajibika katika maendeleo ya mtoto kiakili. Sio tu kiakili bali kimwili kuhakikisha afya yake ya mwili inakuwa imara.
Pia,mzazi unatakiwa kumlisha mtoto na kumfundisha ukuaji wa kiroho.
Kumfundisha na kumpa imani ya kumtegemea Mungu kwani yeye ndiye Muumba wa vitu vyote vijazavyo dunia.

6. Watoto wanahitaji ulinzi na usalama katika maisha yao.
Dunia ya sasa imejaa kila aina ya matukio hivyo basi, ni vema kuwapa ulinzi watoto na kuwahakikishia kuwa duniani ni sehemu salama ya kuishi. Mfano,mtoto pengine aliwahi kuachwa na mzazi mmoja atakuwa anajijengea hisia za woga kuwa hata mzazi aliyekuwa naye ipo siku moja atakuja kumuacha.
Kwahiyo, mtoto atakuwa katika hisia woga na kuhisi duniani hakuna ulinzi na usalama.

7. Wazazi wanatakiwa kuwasaidia watoto kukuza vipaji na zawadi maalumu walizozaliwa nazo.
Mjengee hali ya ndani ya kuridhika kwa kumtia moyo na kumfanya kama vile tayari ameshakamilisha vipaji vyake.
Mhamasishe mtoto katika kile anachopenda. Usiue vipaji vya watoto bali wasaidie kuviendeleza na kuvikuza.

8. Tunaamini kwamba hitaji la mtoto ni upendo kwanza kuliko mahitaji mengine yote.
Mfundishe mtoto kupokea na kutoa Upendo kwa watu wengine.
Mtoto bila chakula atahisi njaa. Na mtoto akikosa upendo utamsababishia njaa ya kihisia na hatimaye atakuwa na ulemavu maisha yake yote.

9. Mama mjamzito huwa anamwathiri mtoto aliyeko tumboni kwa hisia zinazompata mama.
Mama mjamzito akiwa na hisia kama vile furaha na hasira na mtoto hupokea moja kwa moja hisia hizo.
Mtoto anapokuwa mkubwa zile hisia zake zinaanza kujidhihirisha.
Hivyo basi, ni muhimu kwa mama mjamzito kuepuka hisia za huzuni,hasira nk zitakazokuja kumwathiri mtoto baadae.

10. Mzazi anatakiwa kuonyesha upendo kwa mtoto kwa vitendo. Ukweli na uhalisia wa maneno unayomwambia mtoto unapaswa uonekane.
Kama mzazi siku yako ilikuwa ngumu na mambo yako hayajaenda sawa kama ulivyopanga basi ukirudi nyumbani usionyeshe watoto hisia zako.
Kuwa kama hujapatwa na kitu na onesha upendo kwao na siyo matatizo yako yalikukumba.

11. Mtoto anahitaji mguso wa kimwili ( physical touch) kama vile kumkumbatia (hugs) kumbusu (kisses).
Pia,unaweza hata kumshika mkono, mabega,mgongo n.k.
Mguso huu ni aina moja wapo ya mzazi ya kuonesha upendo kwa mtoto wako.
Onesha lugha hii kwa mtoto wako kwani utakua unamkuza vizuri kiupendo naye kisaikolojia atahisi upendo kutoka kwa wazazi wake.

12. Wewe mzazi ndio kiongozi wa mfano au mtu wa mfano “role model” kwa watoto wako.
Mtu wa kwanza wa kumhamasisha mtoto au watoto wako ni wewe mzazi.
Je wewe kama mzazi na mtu wa mfano kwa watoto wako mwenendo wako wa maisha una wabariki watoto wako?
Jibu unalo mwenyewe. Hivyo basi, chukua hatua.

13. Mpe mtoto hongera pale anapofanya kitu chanya.
Mtoto akifanya vizuri shuleni mpe hongera na zawadi ya kumhamasisha zaidi katika masomo

yake.
Kama mtoto amefanya ubunifu wa kitu fulani mpe hongera na endelea kumsaidia kuendeleza ubunifu wake.
Mwisho,hongera huleta nguvu na hamasa katika kupongezwa jambo fulani.

14. Shiriki na watoto michezo mbalimbali kwa kufanya hivyo unakuwa unakuza uhusiano na kuonesha upendo kwao.
Mfano,kama mzazi unaweza kufanya mazoezi na watoto. Kuimba nyimbo mbalimbali na kucheza kwa vitendo kama vile kupiga makofi ,kuruka nk.
Mnaweza kucheza mpira wa miguu pamoja, mpira wa wavu nk.
Kwa kufanya hivyo unakuwa umeshiriki aina ya upendo wa mguso wa kimwili lakini pia zawadi ya muda uliojitolea kwao hufarijika.

15. Kumsifu mtoto,kumfariji na kumpongeza pale anapofanya jambo vema. Mfano, mzazi unaweza kumwambia mwanangu ninakujali,nina kupenda. Watoto ni zawadi kutoka Mungu wapende bila kujali udhaifu wao. Na watoto huwa hawafanani hata siku moja. Hivyo basi, wapatie watoto mtazamo chanya kulingana na udhaifu au ulemavu alionao.

16. Watoto wanahitaji mwongozo katika maisha yao. Watoto wanajifunza kupitia wazazi. Watoto wanaiga kile wanachofanya wazazi huwezi kumkataza mtoto asiangalie televisheni wakati na wewe unaangalia.
Kwakuwa wewe ni kiongozi wa msingi wa watoto wako basi ongoza kwa mfano.
Kama ukisema kitu umaanishe kwa vitendo.

17. Tafuta vielelezo vya kumuonyesha mtoto kama unampenda kwa mfano,unaweza kumuandikia ujumbe mama na baba huwa tunakupenda na ukauweka chumbani kwake au weka sehemu ambayo atauona.
Kama mzazi ni mchoraji basi,chora picha yake ni njia ya kumuonesha upendo. Fanya kitu chochote kumpa imani na matumaini kuwa mtoto wako ana maana kwako.
Uthamini kile alichonacho mtoto.

18. Mjengee mtoto aina nzuri ya kuanza siku yake. Mfano mtoto kabla hajaenda shule unatakiwa kumpa maneno mazuri ya kuanza siku yake na kujiona ni bora na chanya. Kila siku asubuhi mpe neno la hamasa na jioni kaa naye akushirikishe siku yake ilikuwaje.
Kama mzazi unaweza kusafiri andaa ujumbe mzuri wa kumuachia mtoto wa kila siku kulingana na siku ambazo hautakuwepo naye njia hii itamkuza mtoto vizuri sana na kumjengea uwezekano katika maisha yake.

19. Zawadi ya muda kwa mtoto. Watoto wanahitaji uwepo wa mzazi kwa namna mbalimbali kwa mfano, mtoto anapofanya kazi zake za nyumbani anazopewa shule unamsimamia.
Kucheza michezo pamoja, kumfundisha kitu fulani nk.
Unapokuwa na mtoto unatakiwa kumwangalia mtoto machoni yaani kuna takiwa kuwepo na kitu kinachoitwa positive eye contact.
Habari mbaya ni kwamba wazazi wengi wanaangalia watoto wao machoni pale tu wanapofanya makosa. Na tafiti nyingi zinaonesha hivyo wazazi kwenye mitazamo hasi wanawaangalia watoto machoni.
Kaa na watoto wako wape ubora wa muda wako na watazame machoni sio kuangalia pembeni.

20. Unaweza kutumia njia ya kumletea mtoto zawadi kama namna ya kuonesha upendo.
Kama mtoto wako anafurahi pale unakuwa unamletea zawadi zinazoelezea au kuonesha upendo mfanyie pia.
Kila mtoto anakuwa na mambo yake wote hawezi kuwa sawa. Kama mtoto lugha yake ya upendo ni zawadi mtimizie,kama mtoto lugha yake ya kuonesha upendo ni muda fanya hivyo kwa mtoto. Mtoto mwingine anapenda tu jinsi unavyomjali na kumpatia huduma nzuri za malezi.
Mchunguze mtoto wako lugha yake ya upendo na mtimizie kulingana na hitaji lake.

Nakutakia kila la heri katika haya uliyojifunza leo.

Rafiki na mwalimu wako,
Deogratius Kessy
0717101505/0767101504
deokessy.dk@gmail.com
Asante sana

Published by Deogratius Kessy

Mwandishi,mwalimu na mjasiriamali. Unaweza kutembelea Blog yake ya www.kessydeo.home.blog kujifunza zaidi na unaweza kuwasiliana naye kwa namba 0717101505/0767101504 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com

Leave a comment

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

%d bloggers like this: